
SHURA ya Maimamu Tanzania imetangaza hatua za kuikwamisha Rasimu ya
Katiba inayopendekezwa, kwa kwenda kuwaeleza waumini wa dini ya Kiislamu
kupiga kura ya hapana.
Hatua hiyo imekuja baada ya Rasimu ya Katiba inayopendekezwa
iliyowasilishwa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi,
Andrew Chenge, kuiweka kando Mahakama ya Kadhi.Jana mara baada ya
kumalizika kikao cha maimamu wanchi nzima, Msemaji wa Shura ya Maimamu
Tanzania, Sheikh Rajabu Katimba, alisema hatua ya kupiga kura ya hapana
ni moja ya azimio lililoafikiwa na kikao hicho.
“Leo (jana) tulikuwa na kikao kilichojumuisha maimamu wote kutoka
Tanzania na msimamo wetu katika hilo ni hapana,” alisema Sheikh Katimba.
Mbali na msimamo huo, Sheikh Katimba alisema mkutano huo pia umejadili mambo mengine mazito ambayo yatawekwa wazi hivi karibuni.
Sheikh huyo alisema wiki hii watakutana na vyombo vya habari ili kutoa tamko lao rasmi kuhusu Rasimu ya Katiba inayopendekezwa.
Juzi na jana kumekuwa na ujumbe mfupi wa maneno (sms) uliokuwa
ukisambazwa ambao ulisomeka hivi; ‘Assalam Alaykum, ndugu Muislam baada
ya kukataliwa Mahakama ya Kadhi katika mchakato wa Katiba Mpya, Umoja wa
Maimamu Tanzania (SHURA) wanakutana ili kujadili msimamo wa Waislamu
kuipigia kura ya Ndiyo au Hapana mapendekezo ya Katiba Mpya’.
Chanzo kutoka ndani ya kikao hicho ambacho hakikutaka kutajwa jina
lake, kilieleza masuala mengine mbali na azimio hilo la kukwamisha
rasimu hiyo ya Katiba inayopendekezwa.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, kila imamu katika mkutano huo amepewa
jukumu la kwenda kuzungumza na waumini wa msikiti wake na kuwaeleza
ukandamizaji wa Rasimu ya Katiba inayopendekezwa.
“Pamoja na hali hii, lakini kila mmoja wetu sasa tunakwenda kuwasha
moto mikoani maana hili Bunge la Katiba limebeba ajenda zote zenye
masilahi yao kisiasa kuliko hali halisi.
“Kwa hali hii kuanzia sasa unyonge umefika mwisho, maana kila mara
Serikali imekuwa ikitumia ngao ya Watanzania wanyonge hasa Waislamu
kupitisha mambo yao…. Kwa sasa kwa Katiba hii tutaikwamisha tu,”
kilisema chanzo hicho.
No comments:
Post a Comment