kwa mtindo huu Lukuvi lazima ajipange
![]() |
Patrick Ole Sosopi |
YULE
kijana anayetarajia kutoa upinzani mkali kwa William Lukuvi endapo chama
chake Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kitamsimamisha
kuwania ubunge Jimbo la Isimani katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, Patrick
Ole Sosopi amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti Bara wa Baraza la Vijana
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema(BAVICHA). Mbali na kuwa
mbunge wa Jimbo la Isimani kwa awamu ya tatu sasa, William Lukuvi ni
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (sera na uratibu wa bunge). Katika
uchaguzi huo wa BAVICHA uliofanyika jana jijini Dar es Salaam, nafasi
ya Mwenyekiti ilikwenda kwa Patrobasi Katambi na Zeudi Abdalla
alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti Zanzibar.
Kuchaguliwa kwa Sosopi kushika nafasi hiyo nyeti ndani ya chama hicho
kumeelezwa na baadhi ya wafuatiliaji wa siasa za mkoa wa Iringa kwamba
kunamuongezea nguvu kisiasa.
Patrick Ole Sosopi ambaye ni baba wa mke mmoja na mwenye mtoto mmoja,
ni mmasai aliyezaliwa na kukulia mkoa Iringa, jimbo la Ismani.
Ana umri wa miaka 28. Ni msomi wa shahada ya kwanza ya Biashara na
Utawala (rasilimali watu) kutoka chuo kikuu cha Ruaha (RUCO). Kwa sasa
kazi zake ni kufuga ng'ombe.
Historia yake ya uongozi ilianzia akiwa shule ya msingi, sekondari
hadi chuo kikuu cha RUCO ambapo alikuwa waziri wa Fedha kwenye serikali
ya wanafunzi 2011/2012.
Alijiunga rasmi na CHADEMA mwaka 2009 alipokuwa mwanafunzi wa mwaka
wa kwanza akiamini ni chama pekee ambacho kina tija ya kuboresha maisha
ya jamii yake ya kimasai na changamoto mbalimbali ambazo zilikuwa
zikiwakabili.
Aliaminiwa na vijana wa Ismani na kupata kura zote bila kupingwa na
kuwa Mwenyekiti wa BAVICHA jimbo la Ismani. Baada ya kushauriwa na
kushauriana na familia yake na vijana mbalimbali kutoka sehemu
mbalimbali za Tanzania, aligombea nafasi ya Umakamu Mwenyekiti wa
BAVICHA Bara na ameshinda.
Ingawa ni mojawapo wa wasomi wachache kwenye jamii yao ya kimasai, ni
mtu ambaye usomi wake haujamfanya asahau mila na tamaduni za kimasai.
Chakula chake, mavazi yake, desturi yake ya maisha ya kila siku ni
desturi za kwao na zenye kuhuwisha Utanzania.
No comments:
Post a Comment