KAMATI YA WAZIRI WASSIRA YABARIKI ADHABU YA KIFO TANZANIA
LICHA
ya sheria ya kunyonga kupigiwa kelele na jumuiya za kimataifa, wajumbe
wa kamati namba sita ya Bunge Maalumu la Katiba wamependekeza iendelee
kutumika nchini.
Akizungumza
na waandishi wa habari Mjini Dodoma jana, Mwenyekiti wa Kamati hiyo,
Steven Wassira, alisema hali hiyo ilijitokeza wakati wa kujadili Sura ya
nne ya Rasimu ya Katiba.
“Wapo
baadhi ya wajumbe walitaka adhabu ya kifo ifutwe, lakini wengi
walipendekeza adhabu hiyo iendelee, ingawa katika miaka ya hivi
karibuni adhabu hiyo imekuwa ngumu kutekelezeka,” alisema.
Kwa upande wa suala la uraia wa nchi mbili, alisema wameliacha kiporo kutokana na kuwepo kwa mvutano miongoni mwa wajumbe.
Alisema kutokana na hali hiyo, kamati hiyo iliiacha kiporo sura hiyo na kuendelea kujadili sura nyingine.
“Kamati
yetu hadi sasa imejadili sura ya pili, ya tatu na ya nne, Sura ya tano
tuliiacha kiporo, hasa katika suala la uraia pacha,” alisema.
Alisema
suala hilo halikufikia mwisho kutokana na kuwa na mjadala mkubwa
kutokana na wajumbe kugawanyika na kwamba hata hivyo, suala hilo
litapigiwa kura ili kupatiwa majibu.
“Maeneo mengi katika kamati yetu tumekubaliana, lakini yapo maeneo machache ambayo tunatofautiana,” alisema Wassira.
Alisema
pamoja na kujadili sura hizo, kamati yake bado haijapiga kura kupitisha
ibara za sura hizo ambayo kwa mujibu wa sheria inahitajika theluthi
mbili ya wajumbe wote wakati wa kupitisha maamuzi.
Wassira alisisitiza kwamba Bunge la Katiba litaendelea na vikao vyake kama kawaida vya kutunga Katiba.
“Bunge hili haliwezi kuvunjwa kwa sababu watu wachache hawapo, kama ambavyo mnaona tunaendelea na vikao vyetu kama kawaida,” alisema.
No comments:
Post a Comment