Wednesday, September 3, 2014

AFUMWA NA MUMEWE AKIFUNGA NDOA KWA MARA YA PILI NA MUME MWINGINE


MWALIMU mmoja wa Shule ya Msingi Makurumla iliyopo Magomeni jijini Dar es Salaam, Maria Samuel Hoza, amejikuta akiaibika vibaya baada ya mumewe, Bryton Muhanje kumkuta akiwa katika hatua za mwisho za kufunga ndoa nyingine kwenye Kanisa Katoliki la Kigogo Luhanga, Jumamosi iliyopita.
Mwalimu wa Shule ya Msingi Makurumla, Maria Samuel Hoza akiwa katika harakati za kufunga ndoa yake ya pili.

Gazeti hili lilimshuhudia Muhanje, akiingia kanisani na kwenda moja kwa moja mbele ya altare na kumzuia Padri Richard, ambaye alikuwa amemaliza kufungisha ndoa ya kwanza, asifanye hivyo kwa maharusi wanaofuata kwa vile ni batili.

Chanzo chetu makini cha habari kililidokeza gazeti hili juu ya kuwepo kwa mpango wa mwanamke ambaye yupo katika ndoa, kutaka kuolewa tena na mtu mwingine bila mumewe kujua. Kufuatia habari hiyo, kikosi kabambe cha Oparesheni Fichua Maovu kilifanikiwa kupata namba ya mwanaume huyo na kufanya naye mawasiliano ili kujua ukweli wa madai hayo.
Mume wa Maria Samuel Hoza, Bryton Muhanje (kulia) akitoa pingamizi la ndoa ndani ya Kanisa Katoliki la Kigogo Luhanga.
Muhanje alikiri kupata tetesi hizo, lakini alikuwa akihaha kujua sehemu itakakofanyika harusi hiyo na kwamba timu ya vijana wake ilijipanga kuhakikisha anafahamu eneo hilo.Baadaye aliwaeleza OFM kuwa alikuwa alisikia ndoa hiyo ingefungwa Magomeni, hivyo alikodi pikipiki sita zilizofanya doria katika makanisa yote yaliyopo eneo hilo ili kujua mkewe alikuwa kanisa gani.
Pamoja na hivyo, mwanaume huyo pia alikwenda hadi shule anayofundisha mwalimu huyo na kwa kuwa hawamfahamu, alijitambulisha kama ndugu yake na kwamba alikuwa anaomba kujua kanisa ambalo (mkewe) atafunga ndoa, kwani ameelezwa kuwa lipo Magomeni lakini hakuelewa ni lipi.
“Wanafunzi wa pale wakaniambia siyo Magomeni, bali ndoa inafanyika Kigogo Luhanga, ndipo nilipowasiliana na wenzangu na kuwaeleza habari hiyo, nikaongozana na baadhi ya wanafunzi ambao pia walikuwa wanakwenda kwenye harusi hiyo,” alisema.
Padri Richard akitoka nje ya kanisa hilo mara baada ya pingamizi la harusi kutokea.
OFM ikiwa tayari kwa kunasa tukio hilo, walikuwa wameshatinga kanisani hapo mapema na kushuhudia maharusi watatu tofauti wakijiandaa kufunga ndoa, wakiwemo Maria na mwenzake.
Ratiba ilionyesha kwamba ndoa ya wawili hao ilikuwa ya pili, hivyo mara tu zamu yao ilipofika na Padri Richard kuanza kutoa risala ya kuwapongeza kwa hatua waliyofikia, wote walionekana kuwa na bashasha ya siku hiyo muhimu ya kuungana.

Ghafla bila kutarajia, wakati wasaidizi wa padri wakimletea kibakuli chenye pete ya ndoa, Muhanje alijitokeza na kumuomba mchunga kondoo huyo kusitisha zoezi hilo kwa vile anayetaka kufunga ndoa, ni mke wake halali.
Makamanda wa Polisi wakiwa nje ya kanisa tayari ili kutuliza ugomvi.
Akiwa amepigwa na butwaa, padri huyo alilazimkika kwanza kumuuliza bibi harusi kama anamtambua mtu aliyesimama mbele yake, lakini akiwa mkavu alikataa akidai hajawahi kumuona maishani mwake.
Mume akiwa ameongozana na mpambe wake aliyesimamia ndoa yake, alimuomba padri atoe vielelezo kuthibitisha ukweli huo na baada ya kupewa nafasi hiyo, alionesha picha mbalimbali za siku ya harusi yao, nakala ya cheti cha ndoa na akaomba pia aruhusiwe atoe kompyuta yake mpakato ili achezeshe video ya siku hiyo ya Oktoba 29, 2009 alipofunga naye ndoa katika Kanisa la KKT Kimara Korogwe, Dar.

Kwa ushahidi huo, padri huyo alikubaliana naye na kusimamisha zoezi hilo na kuwataka kuongozana kwenda ofisini kwa mazungumzo zaidi. Baada ya mazungumzo marefu ofisini, padri huyo alikubaliana na hoja za mume na hivyo kusitisha zoezi hilo, akidai mwanamke huyo hawezi kuolewa kwa mara ya pili.
Ilifahamika baadaye kuwa Maria, ambaye amezaa mtoto mmoja na Muhanje, alitumia jina la Neema Stanley Hoza katika kusudio lake la kufunga ndoa ya pili.
Baadhi ya wapambe na wanandugu wakirudi makwao mara baada ya ndoa kubatilishwa.
Hata hivyo, wakati kukiwa na sintofahamu ya tukio hilo kanisani, ghafla kikosi cha askari polisi wakiwa katika ‘difenda’ kilitia timu kuhakikisha usalama unakuwepo.Askari hao walisema walipewa taarifa za kuwepo kwa tukio ambalo lingeweza kuhatarisha amani na ili kuhakikisha jambo hilo linatokea, waliondoka na maharusi wa pili baada ya taratibu za kikanisa kukamilika.
Baada ya tukio hilo, Muhanje alisema alimuoa mkewe mwaka huo, baada ya kuwa ameishi naye kinyumba kuanzia mwaka 2005.“Baada ya kukaa naye kwa miaka minne, tukaamua kufunga ndoa mwaka huo wa 2009 na baada ya hapo, yeye akaenda kufanya kazi ya ualimu Lushoto katika Shule ya Shambalai.
Picha ya ushahidi ikionesha ndoa ya halali kati ya Bw. Bryton Muhanje na Mwl. Maria Samuel Hoza.
“Mwanzo tulikuwa na maisha mazuri tu na katika kipindi hicho, nilijitahidi kumfanyia utaratibu wa uhamisho ili aje Dar na kufanikiwa kumleta mwaka 2012 na alipangiwa Shule ya Makurumla.“Baadaye kidogo hali yangu kifedha ikayumba, ndipo matatizo yalipoanza kwani kitendo cha kutegemea hela za mshahara wake katika maisha kikamshinda, akaanza kutafuta visa mbalimbali ili mradi mimi nimpige apate sababu ya kuondoka.
“Alifanya vituko vingi sana, wakati mwingine alifunga mlango na kuondoka na funguo na kwenda kwa dada yake na kulala huko huko, wakati mwingine aliamua tu kuvunja vitu bila kujali hadi mwaka jana mwezi wa nne alipoondoka moja kwa moja kwenda kusikojulikana.“Siku chache zilizopita ndipo nilipopata habari kwamba ana mpango wa kuolewa, ndipo nikaanza kufuatilia ili nijue.

“Nilipokuwa pale kanisani wakati wa kuzuia ndoa, yule mwanaume aliyetaka kumuona mke wangu, alinitishia kuwa atanikomesha, nimeenda polisi kuripoti maana siwezi kujua atafanya nini na nimefungua jalada lenye namba MAG/RB/8452/2014 KUTISHIWA KUUA KWA MANENO.”

No comments:

Post a Comment