Wednesday, September 3, 2014

AMNYONGA MWANAE NA KUMZIKA NDANI YA KIBANDA



Mtoto  mwenye umri  wa mwaka mmoja na miezi miwili , Regina Geofrey ameuawa kikatili kwa kunyongwa  na baba yake mzazi Geofrey Kilngwa ‘Simbaiwe” (27) kwa kuwa alizaliwa  akiwa ameatanguliza makalio yake .
Baba wa  binti  huyo  ambaye pia  ni  mganga wa kienyeji  anayeishi kitongoji cha Mwikang’ombe, kijijicha cha Katuma  ,wilayani Mpanda alitenda unyama huo  kwa madai kuwa mtoto  aliyezaliwa kwa kutanguliza  makalio yake ni mkosi  na nuksi kubwa  katika shughuli zake hizo  za uganga wa kienyeji .
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi , Dhahiri Kidavashari akizungumza na waandishi wa habari amedai kuwa mzazi  huyo  aliyetenda uhalifu huo Julai 20 mwaka huu ambapo alikamatwa na jeshi la Polisi Agosti 26, mwaka huu..
Inadaiwa  siku hiyo ya tukio  mtuhumiwa huyo  baada ya kumnyonga hadi kufa binti yake huyo alimzika kwa siri  katika  kibanda  chake anachofanyia shughuli zake za uganga  wa kienyeji .
Akisimulia mkasa  huo Kamanda Kidavashari alidai kuwa mtoto Regina alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa ambao haukufahamika kwa zaidi ya mwezi mmoja .
“Ndipo  baba mzazi  wa  binti huyo  alipolazimika  kuanza kumuuguza  kwa siri  pasipo mama  yake mzazi kufahamu  kwani alimdanganya kuwa  mtoto  wao  huyo amepelekwa  kutibiwa  na babu yake  huko mkoani Mwanza “ alieleza Kidavashari .
Inadaiwa kuwa  kibanda ambacho  mtuhumiwa alikuwa  akifanyia shughuli  zake  za uganga  kilikuwa mbali na makazi yake hivyo ilikuwa rahisi kumficha mtoto  wake huyo  kwa zaidi  ya mwezi mzima akimtibu  bila mama mzazi  wa mtoto  huyo  kufahamu .
AMNYONGA
Kwa mujibu wa kamanda Kidavashari ,wakazi  wa kitongoji cha Mwikan’gombe  wakiongozwa na  Mwenyekiti wao  walimtilia shaka mtuhumiwa  kutokana na tetesi  zilizozagaa  eneo hilo kuwa  mtoto Regina alikuwa ameuawa na baba yake mzazi  na kuzikwa kwa siri .
Inadaiwa wakazi hao  na mwenyekiti wao  waliamua kufika nyumbani kwa mtuhumiwa  na kuhoji alipo  binti yake Regina ambapo alipinga vikali  lakini alipopekuliwa  kibandani kwake  walibaini kuweko kwa tuta  dogo  lililokuwa  limechimbwa siku za karibuni .
Kidavashari  aliongeza kuwa wakazi hao wakiongozwa na mwenyekiti wao  waliamua kufukua  tuta hilo  na kukuta kichwa cha  mtoto  huyo kisha wakaitaarifu polisi .
Mama ya marehemu aitwae Maria Exavery (22) alidai kuwa hakuhusishwa  wala kupewa  taarifa kwamba binti yake  huyo amekufa “Mie nilikuwa nafahamu kuwa Regina  yuko  kwa  babu yake , Mwanza  akitibiwa “alieleza .
Nae Regina Kaboni (40) mkazi wa Isamilo Mwanza  ambaye alikuwa akitibiwa na mtuhumiwa  anadai  kuwa alishirikishwa katika maziko ya binti huyo
 “Hata hivyo  nilishtushwa sana  kwa kitendo  cha mtuhumiwa kumzika  mwanae  bila ya kumshirikisha mkewe , nilipomuuliza mtuhumiwa  alidai kuwa kwa mila ya kwao  mtoto aliyezaliwa  kwa kutanguliza makalio yake mama mzazi  wa mtoto  ni mwiko kushirikishwa katika maziko ya mtoto huyo ” anadai
Kwa mujibu wa Kidavashari  watu wanne  wakiwemo  wazazi  wa marehemu  wanashikiliwa na Jeshi la Polisi  kwa mahojiano zaidi ambapo watafikishwa  mahakamani mara tu  baada ya upelelezi wa awa;li kukamilika ..
Wengine  wanaoshikiliwa na Jeshi  hilo  ni pamoja na Regina Kaboni na Msolwa Jacob (29) mkazi wa  kitongoji cha Mwikanga’ombe .

No comments:

Post a Comment