MKURUGENZI
wa Kampuni ya Ulinzi ya Advanced Limited, Juma Ntinginya (47) na
wenzake wawili, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa
tuhuma za kuwahifadhi raia wa Nepal.
Washtakiwa
hao walipanda kizimbani jana mbele ya Hakimu Mkazi, Devotha Kisoka na
kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali kutoka Idara ya Uhamiaji,
Patrick Ngayomela.Ngayomela alidai washtakiwa wengine katika kesi hiyo
ni Meneja uendeshaji wa kampuni hiyo, Henry Mwakipunda (34) na dereva
Hamza Sefu (30).Akiwasomea mashtaka yao, Ngayomela alidai kuwa Agosti 29
mwaka huu, maeneo ya Kijitonyama, wilayani Kinondoni, kinyume na
sheria, washtakiwa waliwahifadhi raia wa Nepal huku wakijua kufanya
hivyo ni kosa.
Washtakiwa wote walikiri kutenda makosa hayo na kwamba waliwaingiza raia hao kwa nia ya kufanya kazi katika kampuni yao.
Inadaiwa viza walizokuwa nazo zilikuwa kwa ajili ya kutembea nchini na si kufanya kazi.
Hakimu
Kisoka aliwahukumu washtakiwa kwenda jela mwaka mmoja au kulipa faini ya
Sh 100,000 kila mmoja. Wote walilipa faini na kuachiwa huru.
Wakati
huo huo, mshtakiwa Halit Gurbuz (33) ambaye ni raia wa Uturuki,
alipandishwa kizimbani katika mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi,
Emilius Mchauru, kwa makosa mawili ya kuishi nchini na kufanya kazi bila
kibali.
Ngayomela
akimsomea mashtaka, alidai Agosti 30 mwaka huu maeneo ya Mikocheni,
mshtakiwa akiwa raia wa Uturuki, alikutwa akiishi nchini bila kibali.
Katika
shtaka la pili, anadaiwa huku akijua hana kibali cha kuishi nchini,
alikuwa anafanya kazi Kampuni ya Techno Plus bila kibali cha kumruhusu
kufanya hivyo.
Mshtakiwa
alikiri kosa na Hakimu Mchauru aliahirisha kesi hiyo hadi leo kwa ajili
ya kumsomea hukumu. Hata hivyo, mshtakiwa alikwenda mahabusu Keko.
Komandoo
Sidhee Bahadurkatuwal (kulia) kutoka Nepal akionesha nyumba ya Mrwanda
aliyokuwa akiilinda kupitia kampuni ya Ulinzi ya Advanced Security
karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam,
akiwa na makomandoo wenzake kutoka Nepal.
No comments:
Post a Comment